Poems

Mafuriko

Nitaandika wimbo juu ya mbawa za nzi
Utoe muziki arukapo wausikie walio wengi
Ushairi wa jalalani utaimbwa
Juu ya vidonda vya wakulima
Na usaha ulio jasho lao.
Nitaandika juu ya mbawa za wadudu
Wote warukao
Juu ya mistari ya pundamilia
Na masikio makubwa ya tembo.
Juu ya kuta vyooni, maofisini, madarasani,
Juu ya paa za nyumba, kuta za Ikulu,
Na juu ya khanga na tisheti.
Nitaandika wimbo huu:
Mafuriko ya mwaka huu
Yatishia nyumba kongwe bondeni.
Waliomo wameanza kuihama
Na miti ya umeme imeanguka.
Palipokuwa na mwanga, sasa giza.
Mafuriko ya mwaka huu!
Mti mkongwe umelalia upande
Wa nyumba zetu hafifu.
Upepo mkali uvumapo hatulali.
Kila kukicha twatazama mizizi yake
Na mkao wake, na kuta hafifu za nyumba.
Lazima ukatwe kuanzia matawi hadi shina
Mafuriko ya mwaka huu yaashiria...
Tutabaki kuwasimulia wajukuu:
Mwaka ule wa mafuriko
Miti mingi mikongwe ilianguka.
Mafuriko ya mwaka huu!
Wengi wataumbuka.