Upepo wa Wakati
Juu ya mlima mdogo
Siku moja nilisimama.
Nikatazama chini ziwani, siku
Ya dhoruba. Halafu niliona mawimbi
Yakipanda na kushuka. Yakivimba,
Yakiviringika, yakigongana na kutoa povu
Kama fahari wehu katika bonde lisomajani.
Yalivyotengenezwa!
Yalivyofifia na kuanza tena!
Kamwe sikuona.
Lakini niliyaona yakishuka kwa nguvu
Na kupanda haraka, yakisukumwa
Na upepo wa Magharibi na Mashariki.
Hivyo ndivyo ulimwengu ulivyo.
Na hivyo maisha ya binadamu.
Wanapanda na kushuka
Wakisukumwa na upepo na wakati.
Tazama wanavyojinyakulia madaraka
Kama mzamaji, mguu wa rafikiye, ashikavyo!
Wanavyoshika pesa kama mtoto
Na picha ya bandia
Au asikari mwehu na bunduki yake
Na kutunyamazisha!
Watapanda na kushuka
Na wataanguka kweli!
Wakisukumwa na upepo wa wakati!